Zechariah 8

Bwana Anaahidi Kuibariki Yerusalemu

1Neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote likanijia tena. 2 aHili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Nina wivu sana kwa ajili ya Sayuni, ninawaka wivu kwa ajili yake.”

3 bHili ndilo asemalo Bwana: “Nitarudi Sayuni na kufanya makao Yerusalemu. Kisha Yerusalemu utaitwa mji wa kweli, mlima wa Bwana Mwenye Nguvu Zote utaitwa Mlima Mtakatifu.”

4 cHili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Kwa mara nyingine tena wazee wanaume kwa wanawake walioshiba umri wataketi katika barabara za Yerusalemu, kila mmoja akiwa na mkongojo wake mkononi kwa sababu ya umri wake. 5 dBarabara za mji zitajaa wavulana na wasichana wanaocheza humo.”

6 eHili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Mambo haya yanaweza kuonekana ya ajabu kwa mabaki ya watu wakati huo, lakini yaweza kuwa ya ajabu kwangu?” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

7 fHili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Nitawaokoa watu wangu kutoka nchi za mashariki na magharibi. 8 gNitawarudisha waje kuishi Yerusalemu, watakuwa watu wangu nami nitakuwa mwaminifu na wa haki kwao kama Mungu wao.”

9 hHili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Ninyi ambao sasa mnasikia maneno haya yanayozungumzwa na manabii ambao walikuwepo wakati wa kuwekwa kwa msingi wa nyumba ya Bwana Mwenye Nguvu Zote, mikono yenu na iwe na nguvu ili Hekalu liweze kujengwa. 10 iKabla ya wakati huo, hapakuwepo na ujira kwa mtu wala mnyama. Hakuna mtu aliyeweza kufanya shughuli yake kwa usalama kwa sababu ya adui yake, kwa kuwa nilikuwa nimemfanya kila mtu adui wa jirani yake. 11 jLakini sasa sitawatendea mabaki ya watu hawa kama nilivyowatenda zamani,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

12 k“Mbegu itakua vizuri, mzabibu utazaa matunda yake, ardhi itatoa mazao yake, na mbingu zitadondosha umande wake. Vitu hivi vyote nitawapa mabaki ya watu kama urithi wao. 13 lJinsi mlivyokuwa kitu cha laana katikati ya mataifa, ee Yuda na Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka. Msiogope, bali iacheni mikono yenu iwe na nguvu.”

14 mHili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Kama nilivyokuwa nimekusudia kuleta maangamizi juu yenu, wakati baba zenu waliponikasirisha na sikuonyesha huruma,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, 15 n“hivyo sasa nimeazimia kufanya mema tena kwa Yerusalemu na Yuda. Msiogope. 16 oHaya ndiyo mtakayoyafanya: Semeni kweli kila mtu kwa mwenzake, na mtoe hukumu ya kweli na haki kwenye mahakama zenu, 17 pusipange mabaya dhidi ya jirani yako, wala msipende kuapa kwa uongo. Nayachukia yote haya,” asema Bwana.

18Neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote likanijia tena. 19 qHili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Saumu za miezi ya nne, tano, saba na kumi itakuwa sikukuu za furaha na za shangwe kwa Yuda. Kwa hiyo uipende kweli na amani.”

20Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Mataifa mengi na wakazi wa miji mingi watakuja, 21 rna wenyeji wa mji mmoja watakwenda kwenye mji mwingine na kusema, ‘Twende mara moja na tukamsihi Bwana, na kumtafuta Bwana Mwenye Nguvu Zote. Mimi mwenyewe ninakwenda.’ 22 sPia watu wa kabila nyingi na mataifa yenye nguvu yatakuja Yerusalemu kumtafuta Bwana Mwenye Nguvu Zote na kumsihi.”

23 tHili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Katika siku hizo watu kumi kutoka lugha zote na mataifa, watang’ang’ania upindo wa joho la Myahudi mmoja na kusema, ‘Twende pamoja nawe kwa sababu tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nawe.’ ”
Copyright information for SwhKC